Kauli
ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kwamba mtu
aliyemtolea bastola hadharani Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye si
askari wa Jeshi la Polisi imeibua upya mjadala kuhusu suala hilo.
Waziri
Mwigulu alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza katika kipindi cha
Clouds 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds baada ya
mmoja wa wasikilizaji kutaka kujua kama mtu huyo aliyemtolea bastola
Nape alikamatwa au hajakamatwa.
Baada
ya kauli hiyo, wadadisi wa masuala ya kisiasa wametaka waziri Mwigulu
ambaye Jeshi la Polisi liko chini yake kuueleza umma mtu huyo kama si
askari ni nani au awachukulie hatua askari walioshindwa kumchukulia
hatua mtu huyo.
Nape
alikumbana na kadhia hiyo Machi 23 ikiwa ni saa chache kupita tangu
Rais John Magufuli alipotangaza kumwondoa kwenye Baraza la Mawaziri
akihudumu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Baada
ya kuondolewa asubuhi, siku hiyohiyo mchana Nape alipanga kufanya
mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya Protea jijini Dar es
Salaam ambako alikuta zuio la vyombo vya dola na alipolazimisha
alijikuta akitolewa bastola mbele ya waandishi wa ndani na nje akitakiwa
kurudi ndani ya gari lake na asifanye mkutano huo.
Tangu
kutokea kwa tukio hilo, kumekuwapo mijadala hasa ikilenga kujua kwa
nini hatua hazichukuliwi kwa mtu huyo licha ya video na picha mbalimbali
zinazomwonyesha akitoa bastola na kumnyooshea Nape zipo na zinasambaa
mitandaoni.
Mjadala
huo ulitua katika Bunge la Bajeti lililokutana Aprili na hata katika
mkutano wa Bunge uliomalizika wiki tatu zilizopita mjini Dodoma, baadhi
ya wabunge wakitaka suala hilo na matukio mengine yajadiliwe ndani ya
Bunge jambo ambalo halikufanyika.
Spika
wa Bunge, Job Ndugai alichukua uamuzi wa kuitaka Kamati ya Mambo ya
Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake, Balozi Adadi Rajabu
kulishughulikia suala hilo na taarifa yake ilikuwa isomwe katika mkutano
huo wa Bunge lakini ilishindikana na inatarajiwa kusomwa Novemba.
Juzi,
waziri Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi akijibu swali
la msikilizaji kuhusu mtu huyo kukamatwa au la akisema: “Ninachofahamu
aliyemtishia bastola Nape hakuwa polisi kama ambavyo ilidhaniwa.”
Alisema
katika tukio kama hilo, wahalifu wanaweza kutumia nafasi hiyo kufanya
watakavyo, lakini uchunguzi wa suala hilo unaendelea.
Jana,
gazeti hili lilimtafuta Nape kutaka kujua maoni yake kuhusu kauli ya
waziri Mwigulu ambaye alisema kwa kifupi: “Siwezi kuzungumzia hilo kwani
sijaona… nikiona nitaweza kuzungumza.”
Itakumbukwa,
Aprili 8 mwaka huu, Nape akizungumza jimboni kwake kwa mara ya kwanza
tangu alipoondolewa katika nafasi ya uwaziri alisema hakuchaguliwa
kwenda kuwa waziri bali kuwatumikia wananchi huku akitoa ushauri kwa
Rais Magufuli.
“Namwomba
Rais wangu, na huu ni ushauri tu, simlazimishi, ninampa ushauri na
kumwomba… kwa sababu matendo haya yanamjengea chuki yeye na wananchi kwa
sababu wanadhani yeye ndiye anaowatuma,” alisema.
Nape
alisema, “Sasa ili Rais wangu asijengewe chuki lazima ajiondoe kwenye
jambo hili na namna ya kujiondoa ni kuunda tume iende kuchunguza imletee
ripoti nani yupo nyuma ya haya matendo ya kihuni.”
Alisema,
“Ili atenganishe CCM na matendo ya wahuni wachache wanaotumia dhamana
waliyopewa kuumiza watu na kupoteza watu lazima tume iundwe iende
ikatuletee ukweli, ngoja niseme hapa kwani si nipo nyumbani tu… kama
nilitolewa bastola si ni sawa na kufa tu, basi nipo tayari.”
Atueleze ni nani
Rais
mstaafu wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), John Seka
akizungumza na gazeti hili kuhusu kauli ya waziri Mwigulu alisema
inaashiria kwamba uchunguzi wa suala hilo la Nape umekamilika hivyo
taarifa yake inapaswa kutolewa kwa wananchi.
“Kama
waziri amesema si askari, anawajibu wa kusema ni nani, kwani ushahidi
wa mazingira upo. Lakini kama hakuwa askari alikuwa ni nani, je,
anaruhusiwa kumiliki silaha na je, alitumwa na nani kwa lengo gani,”
alihoji Seka.
Alisema,
“Na kauli hiyo ya waziri inaashiria uchunguzi umekamilika na kubaini
kwamba si askari… nilitarajia jana (juzi) wangemuuliza pale kama si
askari wa Jeshi la Polisi ni nani kwani kwa kauli hiyo uchunguzi
unaonesha umekamilika.”
Alipoulizwa
na gazeti hili kuhusu hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Balozi Adadi Rajabu alisema: “Siwezi
kuyazungumzia masuala hayo katika simu, ‘next week’ nitakuwa bungeni
Dodoma utanitafuta.”
Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mstaafu, Ernest Mangu alisema, “Sina hiyo fursa, waulize walio kwenye nafasi hiyo.”
Alipoulizwa
kwamba anaweza kutoa maoni yake na yakafanyiwa kazi ili huyo
asiyejulikana akajulikana, Mangu alisema, “Kama watahitaji wataniuliza,
wewe unaniuliza kama nani, hayo ni masuala ya kiutendaji.”
Polisi wawajibishwe
Mratibu
wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD), Onesmo ole Ngurumwa
alisema kauli ya waziri Mwigulu inazua utata hasa ikizingatiwa Nape
alizuiwa kufanya mkutano na aliyetoa bastola aliitoa mbele ya askari
wakishuhudia.
“Kitendo
cha yule kutoa silaha mbele ya askari tena na RPC Kaganda (aliyekuwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda) alikuwepo na
akaachwa inaonyesha wanamjua ni mwenzao, kama si mwenzao au hawamjui,
ilikuwaje atoe silaha hadharani na wamwache bila kumchukulia hatua,”
alihoji.
Ole
Ngurumwa alisema, “Kama ndivyo, basi Mwigulu awachukulie hatua askari
wake waliokuwepo wakati huyo asiyejulikana anatoa bastola kwani ni kosa
kutoa silaha hadharani tena mbele ya askari.”
Kauli ya kwanza ya Mwigulu
Itakumbukwa
Machi 24 ikiwa ni siku moja tangu Nape kunyooshewa bastola, waziri
Mwigulu alitumia akaunti yake ya mtandao wa kijamii kuzungumzia sakata
hilo akisema, “Mh. Nape Moses Nnauye sio jambazi, ni Mtanzania, ni
mbunge, mjumbe wa NEC wa CCM, hana record ya uhalifu.”
“Kitendo
cha mtu kumtolea bastola, sio cha kiaskari, sio cha Kitanzania na sio
cha ki Mungu, kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya kamera nawaza
mbali ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini,” alisema.
Alisema,
“Nahusika na usalama wa raia wote wa Tanzania, nimemwelekeza IGP
(Inspekta Jenerali wa Polisi) atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua
kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya uaskari, na kama ni askari basi
sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake,” alisema.

0 comments: