WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee,
Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu amemwelekeza Naibu Katibu Mkuu Tamisemi,
Dk Zainab Chaula kumchukulia hatua daktari wa Hospitali ya Wilaya ya
Maswa, Laurent Biyengo aliyedaiwa kushindwa kuingia kazini na kwenda
kunywa pombe na kusababisha wagonjwa kutopatiwa huduma.
Aidha, Polisi wilayani humo
imethibitisha kumkamata na kumseka ndani daktari huyo kwa maagizo ya
Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Seif Shekalaghe. Hatua imefikiwa baada ya baadhi
ya wagonjwa waliofika katika hospitali hiyo Septemba 27, mwaka huu saa
1:00 hadi saa 3:30 usiku kukosa huduma kutokana na kutokuwepo kwa
daktari huyo wa zamu na kusababisha ujauzito aliokuwa nao Salome John
kutoka na kuharibika wakati akimsubiri daktari huyo aliyekwenda kulewa.
Waziri Ummy ametoa maelekezo hayo kwa
njia ya simu baada ya kupata taarifa hizo kwa njia ya ujumbe mfupi wa
maandishi (SMS) kutoka gazeti hili(Habarileo) juu ya wagonjwa waliofika
kupata huduma katika hospitali hiyo na kumkosa daktari wa zamu.
Wagonjwa waliopatwa na madhira hayo
wakizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa
mkoani Simiyu walisema walifika asubuhi katika hospitali hiyo kwa ajili
ya kupata matibabu, lakini cha kushangaza daktari wa zamu hakuwepo.
Walidai licha ya wauguzi kuwepo, lakini
walishindwa kuwahudumia hasa mjamzito, Salome John aliyekuwa akilia
kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata kwa maelekezo kuwa taratibu
haziruhusu ni hadi hapo watakapoandikiwa cheti na daktari hali
iliyosababisha mgonjwa huyo ujauzito wake kutoka.
“Nilimleta mwanangu akiwa ana mimba mara
baada ya kunieleza ya kuwa anahisi maumivu makali tumbo tulifika
hospitali majira ya saa 1:30 usiku, lakini daktari hatukumkuta licha ya
kuandikiwa cheti lakini tulibaki kumsubiri daktari lakini hakuonekana
ilipofika saa 3:20 usiku maumivu yalimzidi binti yangu na wauguzi
walikataa kutuhudumia hadi tumwone daktari na hatimaye mimba yake
ikatoka,” alidai Suzana Kalumbilo ambaye ni mama mzazi wa Salome.
Kwa mujibu wao, baada ya kuona hali
inazidi kuwa mbaya kwa wagonjwa waliokuwepo walichukua jukumu la
kumpigia simu Mkuu wa wilaya, Dk Shekalaghe ambaye naye alichukua jukumu
la kumpigia simu Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Jonathan Budenu.
Walisema Dk Budenu aliyefika muda mfupi
baada ya kupigiwa simu na DC wake, alifanya jitihada za kupata daktari
mwingine ambaye alifika na kuanza kutoa huduma kwa wagonjwa
waliokuwepo.
Inaelezwa kwamba ilipofika saa 3:40
usiku ndipo Bihengo alipofika akiwa amelewa huku hajitambui na kuingia
katika chumba cha daktari, lakini Mganga Mkuu wa Wilaya, Dk Budemu
alimtoa na kumtaka asitoe huduma yoyote kutokana na hali aliyokuwa nayo.
0 comments: