Ofisi ya Bunge imesema Kiongozi wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe hajanyang’anywa gari.
Taarifa iliyotolewa na Bunge jana Alhamisi imesema kilichotokea ni
kwamba, gari hilo limerudishwa nchini ili dereva afuate utaratibu wa
kupata kibali cha kusafiri nje ya nchi.
Mbowe yuko Nairobi nchini Kenya ambako Mbunge wa Singida Mashariki,
Tundu Lissu anaendelea na matibabu baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa
kwa risasi Septemba 7 akiwa nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.
Bunge limesema ni kweli gari lenye namba ya usajili STL 4587 aina ya
Toyota Prado limetengwa maalumu kwa ajili ya kumuhudumia Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika kutekeleza majukumu yake ya
kikazi na binafsi nchini.
“Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni aliomba gari ikamhudumie
mjini Nairobi nchini Kenya na Ofisi ya Bunge iliridhia ombi hilo na
kuomba taratibu zizingatiwe. Hata hivyo, ofisi iligundua kwamba gari
ilikwenda Nairobi na dereva hakupata kibali cha kusafiri nje ya nchi
ambacho kila mtumishi wa umma anayesafiri nje ya nchi lazima apate
kibali hicho kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi,” imesema taarifa ya Bunge.
Bunge katika taarifa hiyo limesema kwa kuwa utaratibu haukukamilika,
dereva aliambiwa alirejeshe gari hilo nchini na kuliegesha katika Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha hadi utaratibu mwingine utakapokamilika.
“Dereva yupo Dodoma anakamilisha taratibu ili ofisi iweze kumuombea
kibali Ikulu ndipo anaweza kurejea nchini Kenya kwa ajili ya kuendelea
kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,” imesema
taarifa.
Ofisi ya Bunge imesema inasikitishwa kutokana na utaratibu unaotumiwa na
Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa kuzungumzia
masuala yanayohusu ofisi hiyo kupitia kwa msemaji wa chama kama
inavyoonekana kwenye mitandao ya kijamii akitoa malalamiko kwa niaba ya
ofisi hiyo.
“Ni vyema ikaeleweka kwamba Ofisi ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ni kama ofisi nyingine zinazohudumiwa na Sekretarieti ya Bunge
ambayo inapaswa kufuata kanuni na taratibu za uendeshaji wa Ofisi na ni
kosa kwa mtumishi kwenda kinyume na masharti ya Utumishi wa Umma,”
taarifa hiyo imesema.
Imeelezwa katika taarifa kuwa ni dhamira ya Ofisi ya Bunge kuendelea
kumhudumia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kufuata
misingi na kanuni za utumishi wa umma na zile za Bunge bila kuchanganya
na siasa.
“Ofisi ya Bunge inauhakikishia umma kuwa taratibu zikishakamilika
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ataendelea kuhudumiwa popote
atakapokuwa,” imesema taarifa hiyo.


0 comments: