Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali
na viongozi watatu wa Chadema wilayani Malinyi wanashikiliwa na polisi
kwa tuhuma za kufanya kusanyiko lisilo halali.
Mbunge huyo amekamatwa jana Alhamisi
saa 12:40 jioni akitoka kwenye kikao cha ndani cha chama hicho
kilichofanyika katika Kijiji cha Makerere wilayani Malinyi.
Akizungumzia kukamatwa kwa viongozi hao,
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Alfonce Mbassa alisema baada ya
kumaliza kikao, mbunge huyo na viongozi wengine walipanda kwenye magari
ili kuondoka lakini ghafla lilitokea gari la polisi na askari
walimuamuru Lijualikali ashuke.
"Tulishuka wote kujua tatizo ni nini
lakini askari walimhoji Lijualikali kwa nini amekwenda kufanya siasa
Malinyi wakati yeye ni mbunge wa Kilombero," alisema Mbassa.
Alisema walijaribu kuwaelewesha polisi
kwamba kilikuwa ni kikao cha ndani lakini askari walisisitiza kuwa
lilikuwa kusanyiko lisilo halali.
Aliwataja waliokamatwa pamoja na mbunge
huyo kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Malinyi, Emmanuel Lukindo; Katibu
wake, Sadi Lyampawe na Katibu wa Uenezi wa wilaya, Lucas Lyambalimu.
"Lakini tulivyowabana polisi wametuambia wameelekezwa na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Majura Kasika kuwakamata," alisema Mbassa.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo,
mkuu wa wilaya Kasika amesema ni kweli ameagiza polisi kumkamata mbunge
huyo kwa kuwa anafanya siasa nje ya jimbo lake.
"Ndiyo, nimetoa maelekezo akamatwe maana
hakuna mbunge anayeruhusiwa kufanya siasa nje ya jimbo lake na
tunaendelea kumshikilia kwa mahojiano," alisema Kasika.

0 comments: