Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la kila wiki la Raia Mwema kwa muda wa siku 90 kuanzia leo.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk
Hassan Abbasi amesema leo Alhamisi kuwa agizo hilo pia linahusu toleo la
mtandaoni.
Dk Abbasi amesema adhabu hiyo inatokana na toleo namba 529 la Septemba
27 hadi Oktoba 3 lililochapisha habari ya uchambuzi inayosomeka “Urais
utamshinda John Magufuli.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Raia Mwema, Jenerali Ulimwengu amesema wameambiwa sababu ya kusitishwa kwa gazeti hilo ni habari hiyo.
Ulimwengu amesema kwa sasa wanashauriana kuona ni nini cha kufanya.
Dk Abbasi amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kuwa, Serikali
inasisitiza uchambuzi huo ni maoni ya Raia Mwema ya haki (fair
comment), hata hivyo, kwa bahati mbaya, na nia ovu, makala hiyo
ilisheheni nukuu za kutunga na zisizo za kweli zikimsingizia Rais John
Magufuli.
Amesema gazeti hilo pia limewahi kuonywa kwa makosa mbalimbali.
Amesema nukuu za uongo, kutungwa na zenye nia mbaya zikidai Rais alipata
kusema ni, “Suruali za zamani msizitupe, mtazihitaji baadae,” na
“Watakaobaki Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume
kwelikweli.”
Dk Abbasi amesema walipotakiwa kuthibitisha wapi iwe ndani au nje ya
nchi Rais alipata kutoa kauli hizo, wahariri wa Raia Mwema waliomba muda
ambao walipewa. “Wakarejea na kuthibitisha kuwa hawana ushahidi huo,
wakakiri kosa na kuomba radhi.”
Mkurugenzi huyo amesema bado Serikali inaamini Watanzania wakiufanyia
mzaha upotoshaji wa taarifa na uchochezi katika zama hizi za Tehama
amani na utulivu uliopo kwa miaka mingi utapotea na kukaribisha maafa
kama ilivyotokea kwingineko duniani.
“Serikali, katika uamuzi huu, uliochukuliwa kwa mujibu wa mamlaka
aliyonayo Waziri wa Habari katika kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za
Habari Na. 12, 2016, imetoa adhabu ndogo tofauti na ukubwa wa kosa kwa
kuwa wahariri wa gazeti hili hawakufanya tashtiti, wamekiri kosa,”
amesema.
Dk Abbasi amesema kupitia hilo, wamejifunza mambo kadhaa kuhusu
changamoto za kiwango cha weledi wa uandishi wa habari nchini kiasi cha
kuwalazimu kutoa ufafanuzi wa kina kwa faida ya umma na tasnia yenyewe;
kwamba uandishi ni taaluma adhimu na yenye haki na wajibu vinavyopaswa
kufuatwa na si kufanyiwa dhihaka.



0 comments: