Kiongozi mkuu wa chama cha Former Forum
for Democratic Change (FDC) Dk Kizza Besigye amekamatwa leo saa moja
kabla ya Bunge kuanza kujadili pendekezo la kuondoa ukomo wa umri wa
rais.
Besigye, aliyewahi kugombea urais mara nne na akishindwa kwa Rais Yoweri
Museveni alikamatwa mjini hapa alipokwenda kuwahamasisha wafuasi wake
kupinga kufutwa Ibara ya 102 (b) kwenye Katiba iliyoweka ukomo wa
kugombea urais kuwa miaka 75.
Besigye alikataa kushuka kutoka kwenye gari lake hali iliyowalazimisha
maofisa wa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kampala (DPC) wakiongozwa na
Joseph Bakaleke kulivuta gari lake hadi kituoni hapo.
Vilevile Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Fred Mukasa Mbidde
alikamatwa kuhusiana na suala hilo hilo. Zilikuwepo taarifa za kukamatwa
vijana wengi katika maeneo mbalimbali yalikofanyika maandamano ya
kupinga pendekezo hilo. Maeneo mengine yalikofanyika maandamano ni
Mbale, Arua, Mbarara, Masaka na Pader
Katika hatua nyingine, maofisa polisi walisambazwa katika maeneo mengi
muhimu katika jiji la Kampala ulinzi unaohusiana na pendekezo la kufutwa
Ibara ya 102 (b) ya Katiba likilenga kuondoa ukomo wa umri wa rais.
Makao makuu ya ofisi za chama cha FDC yalizingirwa na polisi wa kawaida,
wa kuzuia ghasia na wa kupambana na ugaidi. Ofisi hizo zilizopo
Najjanankumbi katika barabara ya Kampala-Entebbe zimezungukwa na polisi
wenye silaha.
Msemaji wa Polisi Asan Kasingye alisema juzi kwamba maofisa hao
wamesambazwa kwa ajili ya kukabiliana na kitisho cha aina yoyote.
Kadhalika maeneo mengi nyeti, eneo lililojaa shughuli za kibiashara na
Bunge yote yanalindwa.
Polisi wa kijeshi pia wamesambazwa maeneo ya Constitution Square ambako
wameweka mahema sawa na bungeni, eneo muhimu kwa ajili ya mjadala
uliotarajiwa kuwasilishwa jana kuhusu kuondolewa ukomo wa umri.
Kusambazwa kwa wingi kwa askari hao kumefanyika katikati ya kampeni
zinazofanywa na za vikundi vya kisiasa na sasi za kiraia kupinga
marekebisho ya katiba yanayolenga kufuta ukomo wa umri wa rais wa miaka
75. Hoja ya marekebisho hayo ilitarajiwa kuwasilishwa jana baada ya
kushindikana Alhamisi iliyopita.
Mjadala ni mkali ndani ya bunge na chama tawala cha NRM wakiwemo baadhi
ya wenyeviti wa majimbo ambao wamepinga pendekezo la kufuta Ibara ya 102
(b) ya Katiba wakisema ni jaribio la kupindua sheria mama.
Baraza la Viongozi wa Dini nchini limeongeza uzito kwa kutoa wito kwa
serikali kuruhusu hoja ya ukomo wa umri wa rais iamuliwe na wananchi
wote kwa kupiga Kura ya Maoni.
Baraza hilo linalojumuisha wakuu saba wa madhehebu makubwa ya dini
nchini limesema katika taarifa yao ya pamoja wiki iliyopita kwamba watu
waruhusiwe kuamua hatima yao.
“Mjadala kuhusu kuondolewa kwa ukomo wa umri wa rais si suala la upande
mmoja ambalo linahodhiwa na wanasiasa na au wabunge...wananchi wana
maoni tofauti kuhusu sauala hilo, hivyo kuna haja ya kusikiliza kwa
utulivu pande zote bila ya kuegemea upande mmoja na kuutisha mwingine.
Hivi karibuni wabunge wa chama tawala cha National Resistance Movement
(NRM) na wa kujitegemea walipitisha uamuzi wa kuondolewa ukomo wa umri
wa miaka 75 uliowekwa katika Katiba.
Ikiwa marekebisho hayo yatapitishwa bungeni, itakuwa na maana kwamba
Rais Museveni mwenye umri wa miaka 73 sasa ataweza kugombea uchaguzi
ujao mwaka 2021 akiwa na umri wa miaka 77. Mwaka 2005, katiba ilifanyiwa
marekebisho ukaondolewa ukomo wa mihula miwili ya miaka mitano kila
mmoja

0 comments: