Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema
hajapelekewa uthibitisho kuhusiana na maiti za wanaume watatu waliokutwa
pembezoni mwa Bahari ya Hindi eneo la Coco Beach.
Amesema kwamba iwapo atapelekewa udhibitisho huo ni lazima atatolea ufafanuzi suala hilo kiundani zaidi.
Maiti za watu hao zilikutwa juzi Septemba 24 ambapo mbili zilifungwa
kwenye viroba huku nyingine zikiwa ikiwa imekutwa na jiwe kubwa
lililofungwa na kamba.
“Sijaletewa ‘fact’ nikiletewa nitalitolea ufafanuzi,”amesema Mambosasa.
Wafanyabiashara wa mihogo wa eneo hilo wamesema wakiwa kwenye biashara
zao asubuhi ghafla waliona maiti moja ikielea karibu na miti aina ya
mikoko ikiwa na jiwe lililofungwa kifuani huku mikono yake ikifungwa na
kamba.
Mmoja wa wafanyabiashara, Aziza Ally amesema baada ya kuona maiti hiyo
walitoa taarifa polisi ambapo walifika saa 4 asubuhi na kuichukua kwenye
gari lao.
Amesema ilipofika saa 8 mchana waliona maiti mbili kila moja ikiwa
kwenye kiroba zikielea ndipo mmoja wao alipoamua kutoa taarifa polisi
baadaye zikachukuliwa.
"Polisi walipokuja kuchukua hizi maiti hakuna hata mtu mmoja
aliyeruhusiwa kusogelea na kupiga picha tulishangaa sana kuona ulinzi
mkali tofauti na siku zote na aliyebainika amepiga alipokonywa simu
yake," amesema Ally.
Mfanyabiashara mwingine Issa Isaya amesema cha kushangaza maiti zinazookotwa ni za kiume pekee.
Amesema wanaishi kwa wasiwasi kwasababu kila wiki wanakuta maiti zikiwa zinaelea kwenye maeneo hayo.

0 comments: