
Serikali kupitia wakala wake wa ujenzi nchini (TBA) imetoa msaada wa
nyumba kwa askari polisi waliounguliwa nyumba zao hapo jana, mpaka pale
watakapopata makazi rasmi.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Charles
Mkumbo , ambapo amesema baada ya ajali hiyo askari hao walikosa mahali
pakuishi, hivyo wanaishukuru TBA kwa msaada huo.
"Ule moto umeteketeza kila kitu kabisa, hivyo wale askari hawakuwa na
sehemu ya kuishi, jana tuliwahifadhi kwenye bwalo letu la polisi, lakini
leo wamepatiwa msaada na wakala wa ujenzi wa serikali (TBA ), wamepewa
nyumba za kuishi kwa muda hadi pale watakapopatiwa makazi rasmi,
tunashukuru kwa hilo", amesema Kamanda Mkumbo.
Tukio la kuteketea kwa nyumba hizo limetokea usiku wa Septemba 27 mwaka
huu majira ya saa mbili na kuteketeza nyumba hizo, lakini jeshi la
zimamoto liliwahi eneo la tukio na kutoa msaada kwa wananchi ambao
walianza kuzima.
0 comments: