Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Usalama wanaendelea kuchunguza tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mh. Tundu Lissu lililotokea Septemba 7 mwaka huu huko nyumbani kwake Area D, Dodoma.
Akizungumza katika kituo cha Televisheni cha Clouds 360 asubuhi leo, Waziri Nchemba amesema kuwa walitamani Dereva wa Lissu ahojiwe mapema ndio maana Polisi Dodoma walitoa wito afike kuhojiwa lakini ziko taarifa kuwa Dereva huyo anapatiwa matibabu Nairobi Kenya. Hata hivyo Waziri Mwigulu amesisitiza kuwa Dereva huyo anasubiriwa akimaliza matibabu ili ahojiwe na Polisi.
Aidha, Waziri Nchemba amesema kuwa, kufuatia tukio hilo tayari magari 10 yanayofanana na lililohusika na shambulio la Lissu yamekamatwa kwa upelelezi. Waziri Mwigulu amekaririwa akisema tayari mamlaka inazo taarifa nyeti juu ya tukio hilo hivyo amewataka Watanzania kuwa watulivu katika kipindi hiki ambapo Jeshi la Polisi wanaendelea na Uchunguzi, ” Kuna taarifa nyeti tunazo, Watanzania wawe na subira” amesema Waziri Nchemba akiongeza kuwa baada ya upelelezi mdogo wa Ofisi ya DCI imebainika Gari iliyodaiwa kumfuatilia Lissu ni gari ndogo iliyoko Mkoani Arusha.
Akifafanua zaidi matukio mbalimbali ya kihalifu yaliyopata kutokea Nchini kama kifo cha Mchungaji Mtikila aliekuwa Mwenyekiti wa DP Taifa aliefariki kwa ajali ya gari mwaka juzi na Alphonce Mawazo aliekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Waziri Mwigulu amesema kuwa sasa Serikali inaandaa mpango wa kuhakikisha kila tukio linatolewa ufafanuzi mapema ili kutoruhusu watu kuzusha taarifa zinazoweza kupotosha umma. Kuhusu Ben Saanane Waziri amesema kuwa si rahisi kusema amekufa ama yuko hai kwa sababu Polisi bado wanaendelea na uchunguzi.
Pia Waziri Mwigulu amesema anawachukia sana watu wasiojulikana na kukimbilia kusikojulikana. Akikumbushia tukio la kutolewa Bastola Mbunge Nape Nnauye, Waziri amesema kuwa mtu aliemtolea Bastola Mbunge Nape si Askari wa Jeshi la Polisi na hakuwa amevaa sare hivyo ni vigumu kumtambua.
0 comments: