
Mtu mmoja wa Kigamboni, amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusambaza
ujumbe katika mtandao kwamba kachero wa Usalama wa Taifa ameonekana
jijini Nairobi karibu na hospitali aliyolazwa Mbunge wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu.
Mshtakiwa huyo Mbutusyo Mwakihaba (40), amefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa shtaka linalomkabili mbele ya Hakimu
Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.
Wakili wa Serikali Janeth Magoho alidai mshtakiwa anakabiliwa na kosa la
kusambaza taarifa za uongo chini ya kifungu namba 16 cha Sheria ya
mtandao namba 4 ya mwaka 2015.
Janeth amedai Septemba 11, mwaka huu kupitia mtandao wa ‘WhatsApp’
mshtakiwa aliandika “Huyu ni Kachero wa Usalama wa Taifa anatambulika
kwa jina la Jose anaonekana Nairobi karibu na hospitali alikolazwa
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu…Mwaxcheni mwenzenu”.
Mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo, upelelezi wa kesi haujakamilika
ambapo Hakimu Nongwa alikubali kumpa dhamana kwa masharti ya kuwa na
wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini dhamana ya Sh milioni tano
kila mmoja ambapo mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo na
kurudishwa mahabusu hadi Oktoba 12, mwaka huu.
0 comments: